UMUHIMU WA KUWEKA IMANI YAKO KATIKA
JINA LA YESU KRISTO
“Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa Na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango WA hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu.” (matendo ya mitume 3:1-8)
Ukifuatilia historia ya kilema huyu aliyeponywa utaona ya kuwa alikuwa hivyo tangu kuzaliwa, na alipopona alikuwa na umri uliopita miaka arobaini (matendo ya mitume 4:22)
Siri ya muujiza huu ilikuwa ni nini? Je! Kilema huyo alipona kwa uwezo wa petro na yohana au kwa uweza wa Jina la Yesu Kristo! Nauliza maswali haya kwa kuwa watu wengi wakiona mtu anatumiwa na Mungu katika uponyaji wanaweka imani zao kwa huyo mtumishi badala ya kuweka imani zao katika Jina la Yesu Kristo!
Na ndivyo ilivyokuwa wakati kilema huyu alipopona, watu waliokuwa hekaluni waliwashangaa akina petro na yohana kama vile kilema alipona kwa uwezo wao. Petro alipoona hali hiyo aliamua kuwaeleza watu haoukweli ulivyo, akasema; “Basi alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi?” (Matendo ya mitume 3:11-12).
Petro alikuwa anafanya jambo muhimu hapakwa kusaidia kubadilisha mawazo ya watu ya kufikiria kuwa uwezo uliomponya yule kilema ulikuwa ni wa petro na yohana ambayo haikuwa kweli. Kama uwezo huu haukuwa wao, muujiza huu siri yake ni nini? Petro aliendelea kusema hivi, “Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote.” (Matendo 3:13-16)
Hebu tafakari maneno haya ya petro, “Na kwa IMANI KATIKA JINA LAKE, JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU…” wakina petro na yohana waliweka imani zao katika Jina la Yesu Kristo. Walikuwa na uhakika mioyoni mwao kuwa siri ya muujiza imo katika jina la yesu kristo – ndiyo maana walopomkuta huyo kilema walimwamuru asimame kwa jina hilo!
Weka imani yako katika Jina la Yesu Kristo ukitaka kuona ishara na miujiza ya Yesu Kristo maishani mwako na kwa wale unaowahudumia. Wakijua hili wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo walipokatazwa kuwa wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu Kristo na kuhani mkuu Anasi, waliomba wakisema, “….Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa JINA LA MTUMISHI WAKO MTAKATIFU YESU.” (matendo 4:18,29-31)
Ni muhimu kuwaeleza watu umuhimu wa kuweka imani zao katika Jina la yesu Kristo wakitaka kuona mkono wa Bwana ukiponya na kuokoa, ukifanya ishara na miujiza.
Nakumbuka kuna mama mmoja alifika nyumbani kwangu akiwa anaumwa sana toka nje ya mkoa huu wa Arusha ninaokaa. Baada ya mahojiano naye nilifahamu ya kuwa ameugua bila kupona kwa muda wa miaka miwili. Na katika hiyo miaka miwili amezunguka kwa watu mbalimbali kuombewa bila mafanikio. Alipoona haponi akaenda kwa waganga wa kienyeji ambako nako hakupona. Alipoona kwa waganga wa kienyeji haponi, akaanza kutafuta watumishi tena ili wamwombee.
Katika mazungumzo hayo nilitambua kuwa anapokwenda kuombewa anaweka imani yake katika watu wanaomwombea na wala haweki imani yake katika jina la Jina Yesu Kristo.
Nilifungua biblia yangu na nikaanza kuzungumza naye juu ya uweza wa jina la Yesu Kristo, na umuhimu way eye kuweka imani yake katika jina la , na umuhimu wa yeye kuweka imani yake katika jina la Yesu Kristo na siyo kwangu. Mwishoni nikamwuliza kama ameelewa na ikiwa yuko tayari kwa maombi kwa kulitumia jina la Yesu Kristo. Yule mama akajibu akasema; “ndiyo nipo tayari kwa kuombewa, naamini kwa jina la Yesu Kristo nitapokea uponyaji”
Mara nilipoanza kuomba, aliangushwa chini na mapepo yaliyojidhihirisha toka ndani mwake. Nikayaamuru mapepo hayo yamtoke yule mama kwa Jina la Yesu Kristo- na mara hiyo yakamtoka yule mama na akawa mzima.
Ugonjwa uliomsumbua kwa muda wa miaka miwili ulitoweka, yule mama pamoja na mume wake aliyemsindikiza waliondoka kwa furaha huku wakimsifu Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea. Kumbuka petro alisema, “kwa IMANI KATIKA JINA LAKE (YESU), JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU…”
ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAPONYWA
Nabii Yoeli alitabiri kuwa, “Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana. (yoeli 2:32)
Mtume Paulo alitilia mkazo unabii huu aliposema,
“Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka” (warumi 10:12-13).
Kila anayeliitia Jina la Bwana Yesu kwa imani anaponywa na, anaokoka kwa kuwa ndani ya jina hili la Yesu Kristo mna uponyaji na wokovu kwa kila amwaminiye Yesu Kristo.
Lakini mtume Paulo anauliza swali muhimu, ambalo ni muhimu kulitafakari, anasema, “Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?” (Warumi 10:14)
Hili jambo ni kweli. Huwezi kumwita mtu usiyemwamini. Hii ina maana ya kuwa ikiwa tunataka watu waliitie jina la Yesu Kristo ili waokoke na kuponywa madhaifu yao, inatubidi tufundishe na kuhubiri juu ya Yesu na jina lake.
Ndiyo maana Bwana Yesu Kristo alimwambia anania ya kuwa Paulo “ni chombo kiteule kwangu, ALICHUKUE JINA LANGU mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.” (Matendo ya mitume 9:15).
Biblia inasema pia kuwa, “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, AKAWAHUBIRI KRISTO. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia Kwa sauti kuu; Na watu wengi waliopooza, Na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule” (matendo 8:5-8)
Smith Wigglesworth aliyekuwa mhibiri wa inili nchini uiengereza miaka ya 1930 aliwahi kushuhudia katika mahubiri yake kuwa siku moja aliitwa kwenda kumuombea mgomjwa mmoja wa kifafaaliyekuwa amezidiwa hata kushindwa kuamka. Anasema watu wa eneno lile hata ndugu zake yule mgonjwa walikuwa wamekata tama. Waliona ndugu yao atakufa kwa ugonjwa huo, kwa hiyo ilimchukua muda Bwana Smith Wigglesworthkupata walio tayari kushirikiana naye katika kumwombea mgojwa yule.
Mwishowe alifanikiwa kuwapata na anasema walikizunguka kitanda cha yule mgonjwa na wakaanza kuliitia Jina La Yesu kwa pamoja wakisema “Yesu, Yesu, Yesu…” kwa kulirudia rudia jina hili. Baada ya kulitia jina la Yesu kwa muda hivi, anasema nguvu za Mungu zilishuka kitandani mwa yule mgonjwa, zikamtingisha mgonjwa na kitanda chake.
Yule mgonjwa akapona saa ile ile, akavaa nguo na kutoka nje. Kijiji kizima kilitaharuki na kushangaa kilipomuona mtu yule amepona. Smith Wigglesworth alipoona watu wamekusanyika hivyo wakishangaa, alichukua Biblia yake akahubiri, na watu wengi waliokoka na kutubu siku ile.
Ni muhimu ufahamu kuwa muujiza unaofanyika kwa Jina la Yesu Kristo unawavuta watu kwa Yesu Kristo, wamwamini na kumfuata. Ndiyo maana imeandikwa juu ya Yesu Kristo kuwa;
“Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya” (yohana 2:23)
siku moja nilikuwa katika sehemu Fulani nikifundisha juu ya Jina La Yesu Kristo. Mwisho wa somo nilisema wanaotaka kujazwa na Roho Mtakatifu na wanene kwa lugha mpya pamoja na wagonjwa waje mbele. Watu wengi walikuja mbele.
Niliwaambia kuwa hatutaomba neno lolote zaidi ya kuliitia jina la Yesu kwa pamoja na kwa kulirudia rudia. Kwa pamoja tukaanza kuliitia jina la Yesu tukisema kwa sauti, “Yesu, Yesu, Yesu….”
Muda haukupia mwingi tukiwa bado tunaliitia Jina hili nikasikia toka upande wangu wa kushoto sauti ya mengi yakiporomoka. Nilijua hii ni ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifukwani mahali tulipokuwa hakukuwa na mto wowote karibu, wala mvua ilikuw hainyeshi. Baadaye nilipowaeleza watu juu ya sauti hiyo ya maji mengi, kuna wengine waliosema kuwa pia waliisikia.
Tulipoendelea kuliitia Jina la Yesu Kristo, wagonjwa walipona, waliokuwa na mapepo walifunguliwa, na wengine walijazwa Roho mtakatifu na kuanza kuzungumza kwa lugha mpya! Ishara na miujiza mingi ilifanyika kwa Jina la Yesu Kristo!
Kumbuka Yesu Kristo alisema, “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya” (marko 16:17-18).
HUKUMU KWA KUTOLIAMINI JINA LA YESU
“Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu” (yohana 3:18)
Usipoliamini jina la mwana pekee wa Mungu – jina la Yesu Kristo ujue umekwisha kuhukumiwa. Hii ina maana unapoteza Wokovu, unapoteza ushindi na uzima wa milele unaopatikana ndani ya Yesu Kristo nab ado unakaa katika mauti! Hebu soma na kutafakari mistari ifuatayo ili uone umuhimu wa kuliamini jina la Yesu Kristo:
“Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri Kwa Mungu; Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, Kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba TULIAMINI JINA LA MWANA WAKE YESU KRISTO, Na kupendana sisi Kwa sisi, kama alivyotupa amri”. (1 yohana 3:21-23)
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo WA kufanyika watoto WA Mungu, ndio wale WALIAMINIO JINA LAKE” (yohana 1:12)
“Kwa maana kila kitu kilichozaliwa Na Mungu huushinda ulimwengu; Na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, Ili mjue ya kuwa mna uzima WA milele, ninyi MNAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU.” (1 yohana 5:4-5; 11-13)
“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, Kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” (Matendo ya mitume 4:12) – Isipokuwa ni Jina la Yesu Kristo pekee. Ndio maana biblia inasema hivi katika kitabu cha Matendo ya mitume 2:21, “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana (Yesu Kristo) ataokolewa”.
Muhimu
Kama nilivyokwisha kukuandikia katika sura ya tatu ya somo hili – ukitaka kulitumia jina la Yesu Kristo kihalali na uweze kuona uwezo na mamlaka yake ni muhimu ,
Kwanza: uwe mwana wa Mungu kwa kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama Bwana na mwokozi wako; maana yake uokoke! Unapookoka unafanyika mrithi pamoja na Kristo (warumi 8:16-17).
Pili: uwe mtii ukifuata maagizo ya Neno la Kristo katika Roho mtakatifu.
Kuna watu wengine wanataka kuwa watii kufuata maagizo ya Neno la Mungu huku hawapendi kuokoka. Hawajui utii bila kuokoka ni utii nusu – ukitaka uone uweza mkuu wa jina la Yesu Kristo katika maisha yako inabidi ufanye yote mawili – uokoke na utii.
Ikiwa hujaokoka na unataka uokoke sasa isome na kuikiri sala ifuatayo kwa sauti (ikiwezekana upige magoti) mahali pa utulivu huku ukiamini ya kuwa Mungu anakusikia.
“Ee Mungu mtakatifu, nimesikia Neno lako name nimeamini. Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu yote. Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa ajili yangu, naomba initakase sasa, katika roho yangu, nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu sasa; ee Bwana Yesu nakuomba uingie ndani yangu, uwe Bwana na mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa kunisamehe dhambi zangu zote na ahsante kwa kuniokoa. Amina.”
Ikiwa umeikiri sala hii kwa imani, basi tabua kuwa Bwana Yesu kristo amekusamehe dhambi zako na kukupa Wokovu. Dhambi zako zimesamehewa na Mungu na kusahauliwa kama ilivyoandikwa katika neno lake (Isaya 1:18). Ni muhimu utafute kanisa LA WATU WALIOMPOKEA Yesu Kristoili uweze kuukulia Wokovu na kujifunza mambo mengi zaidi.
Jina la YESU KRISTO ni halali yako kulitumia.
Ukipenda unaweza kutuandikia mimi na mke wangu kwa anwani yetu iliyi nyuma ya kitabu hiki juu ya uamuzi huu ulioufikia leo wa kuokoka; ili tumshukuru Mungu pamoja. Pia tuweze kukuombea zaidi nakukutumia mafundisho zaidi.
mwisho. kitabu hiki kiliandikwa na mtumishi wa Mungu Christopher Mwakasege
Amen
ReplyDeleteNIMEBARKIWA SANA KWA MAFUNDISHO MAZURI SANA ,MUNGU AENDELEE KUKUTUMIA ILI WATU WAPATE WOKOVU WA KWELI
ReplyDeleteNimejifunza kitu
ReplyDelete