Sura ya Kwanza
JINA LA YESU KRISTO – MOJAWAPO YA FUNGUO ZA UFLME WA MBINGUNI.
“Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; Na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; Na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” (mathayo 16:16-18)
Maneno haya ya Yesu Kristo yanatuonyesha kuwa, nia yake ni kulienga kanisa lililo na mamlaka kuliko shetani. Kanisa ni mwili wake (waefeso 1:22-23). Wakristo waliookolewa kwa damu ya Yesu Kristo ni viungo vya mwili wa Kristo – ni viungo vya kanisa (1korintho 12:12,13,27). Kwa hiyo Yesu Kristo anaposema atalijenga kanisa lake wala milango ya kuzimu haitalishinda – ana maana ya kuwa, kila mkristo aliye wake anajengwa kiroho awe na mamlaka ya kumshinda shetani.
Ni budi tufahamu ya kuwa, Yesu Kristo hawezi kutuambia tufungue kama hakuna kitu cha kukifungua. Hawezi kutuambia tufunge kama hakuna kitu cha kufunga. Kwa hiyo ni lazima kuna vitu vya kuvifunga na kuna vitu vya kuvifungua. Pia tufahamu kuwa, Yesu Kristo hawezi kutuambia tufunge na kufungua kabla hajatupa uwezo na mamlaka ya kufanya hivyo. Uwezo na mamlaka tunapata ndani ya Kristo aliyetukabidhi funguo za ufalme wa mbinguni.
Itakuwa haina maana kwa Yesu Kristo kutukabidhi funguo bila ya kutufundisha namna ya kuzitumia. Hawezi kutukabidhi mamlaka bila ya kutufundisha namna ya kuyatumia. Yesu Kristo anasema tukifunga au tukifungua, mbinguni nako kunatia mhuri kitendo hicho. Hatuwezi kufanya hivyo kama tulichokifanya hakifanani na mapenzi yake. Ndiyo maana tunaomba kuwa mapenzi yake yatimizwe hapa duniani, kama yanavyotimizwa huko mbinguni. Kwa maneno mengine tunaweza kusema ya kuwa ukifanya kitu chochote katika mappenzi ya Mungu, Ufalme wa mbinguni utakuwa upande wako.
Aina za Funguo
Biblia inazungumza juu ya funguo za aina zisizopungua nne zifuatazo:
1. Funguo za ufalme wa mbinguni – mathayo 16:19 – Yesu Kristo amekabidhi funguo hizi kwa kanisa (wakristo).
2. Funguo za mauti na kuzimu – Ufunuo 1:18 – Funguo hizi anazo Yesu Kristo – baadaye atampa malaika mmoja funguo za kuzimu amfunge Ibilisi (ufunuo 20:1-3)
3. Ufunguo wa nyumba ya Daudi – Isaya 22:22; ufunuo 3:7
4. Ufunguo wa kawaida wa mlango – waamuzi 3:25
Neno ufunguo lililoandikwa katika mathayo 16:19; ufunuo 1:18; Isaya 22:22; na ufunuo 3:7 lina maana ya ‘mamlaka’. Kazi ya funguo ni kufunga na kufungua. Kwa hiyo ukipewa funguo maana yake umepewa mamlaka ya kufunga na kufungua.
Kwa mfano, mtu akikupa funguo za chumba- maana yake una mamlaka juu ya chumba hicho kukifunga na kukifungua. Mtu yeyote akitaka kuingia kwenye chumba hicho hawezi kufanya hivyo bila kupata ruhusa kutoka kwako ya kumfungulia. Ukipewa funguo za gari maana yake kwa muda huo ambao una funguo hizo za gari, una mamlaka juu ya hilo gari kulifunga lisitumike au kulifungua litumike. Mtu akitaka kulitumia ni budi aje kwako kwa ajili ya kufuata funguo.
Kwa hiyo Yesu Kristo aliposema ametupa funguo za ufalme wa mbinguni alikuwa ana maana ya kuwa ametupa ‘mamaka’ ya ufalme wa mbinguni. Ni vizuri ufahamu hapa ya kuwa ufalme wa mbinguni ni ufalme wa Mungu ulio na mamlaka juu ya falme nyingine kama vile ufalme wa shetani, ufalme wa wanyama, ufalme wa wadudu, ufalme wa mimea, falme za wanadamu, ufalme wa ndege, na kadhalika. Ikiwa wewe ni mkristo uliyeookoka basi fahamu ya kuwa, una mamlaka uliyopewa na Yesu Kristo juu ya falme hizi!
Yesu Kristo anaendelea kusema kuwa, “lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa na mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
Kwa mfano, ukiamua kumfunga Ibilisi asikusumbue katika maisha yako, mbinguni pia wanasimamia utekelezaji wa jambo hili. Hata kama Ibilisi ataamua ‘kukata rufaa’ juu ya uamuzi wa kumzuia asikusumbue na akaenda kwa MUngu kuomba aachiliwe – Mungu atamwambia ‘rudi kwa aliyekufunga, akikufungua name nitakufungua, lakini asipokufungua name sikufungui’.
Unaweza kusema mbona shetani alipewa ruhusa na Mungu kumjaribu Ayubu. Kumbuka kuwa Ayubu aliishi katika agano la kale na sisi tunaishi katika agano jipya ambalo ndani yake tuna mamlaka ya kumfunga shetani kwa jina la Yesu Kristo.
Kuna wakristo wengi wameonewa na Ibilisi kwa kuwa hawajui mamlaka waliyo nayo na namna ya kuyatumia. Jambo lingine ninalotaka uoe hapa ni kwamba Yesu Kristo alisema ametupa “funguo za ufalme wa mbinguni”, na hakusema ametupa ufunguo wa ufalme wa mbinguni. Neno hili “ZA” lina maana yakuwa kuna funguo za ufalme wa mbinguni zaidi ya moja. Kumbuka kuwa kuna tofauti ya funguo za ufalme wa mbingui na zile funguo za mauti na za kuzimu.
Funguo za mauti na za kuzimu alikuwa nazo shetani hadi aliponyang’anywa funguo hizo na Yesu Kristo kwa kufa kwake msalabani na kufufuka. Funguo za mauti na za kuzimu anazo Yesu Kristo sasa.
Funguo za ufalme wa mbinguni anazo Yesu Kristo lakini amezikabidhi kwa wakristo waliomo duniani wazitumie. Ukifuatilia maneno yaliyomo katika agano jipya utaona ya kuwa kuna funguo nne za ufalme wa mbinguni nazo ni:
1. Jina la Yesu Kristo
2. Damu ya Yesu Kristo
3. Neno la Yesu Kristo
4. Nguvu za Roho mtakatifu
Katika kitabu hiki tunajifunza juu ya jina la Yesu Kristo ambalo ni mojawapo ya funguo za ufalme wa mbinguni.
Tumia mamlaka uliopewa.
Kuna wakati fulani ambapo nilihangaika siku nyingi kwa kuomba na kwa kulia usiku na mchana ili shida niliyo kuwa nayo iniondoke bila mafanikio. Nilikuwa naomba kwa Mungu, lakini sikuona mabadiliko yoyote, ilikuwa kama vile Mungu ameziba masikio yake asisikie maombi yangu. Pamija na maombi niliongeza kulia zaidi lakini sikufanikiwa pia.
Nikiwa katika hali ya kukata tama huku nikijiuliza kwa nini naomba kwa Mungu lakini shida iliyonisumbua haiondoki – Roho mtakatifu alisema ndani yangu ya roho yangu maneno haya, “shida yako inayokusumbua inaletwa na shetani. Unayo mamlaka ya kumkemea shetani naye ataondoka na shida uliyonayo itakwisha. Kama hufahamu juu ya mamlaka uliyonayo soma vitabu vya waefeso, wafilipi, wakolosai na vitabu vingine katika biblia”.
Niliposikia maneno hayo nikaomba tena, “ee Bwana unifundishe juu ya mamlaka uliyonipa ili nipate kuitumia.” Namshukuru Mungu ya kuwa alisikia sala yangu na alianza kunifundisha juu ya mamlaka aliyoipa na bado anaendelea kunifundisha hatua kwa hatua kila siku.
Nilipoendeklae kujifunza ndipo nilipotambua ya kuwa si kila shida uliyonayo itaondoka kwa maombi, bali shida nyingine zinaondoka kwa KUAMURU katika Jina la Yesu Kristo shida hiyo iondoke au kwa KUAMURU hali unayoitaka itokee.
Kwa hiyo siku moja usiku niliamua kutumia mamlaka niliyonayo katika Jina la Yesu Kristo ili shetani aondoke katika eneo alilokuwa ananiletea shida – mara hiyo hiyo kulitokea mabadiliko. Shida iliyonisumbua kwa muda mrefu ilitoweka mara moja. Badala ya kusubiri Mungu afamye kitu kwanza juu ya shida hiyo, niliamuru iondoke na Mungu akasimamia utekelezaji wake!
Ndivyo alivyomaanisha aliposema, “lolote utakalolifunga(wewe) duniani, litakuwa limefungwa mbinguni” – maana yake Mungu atausimamia uamuzi wako wa kulifunga hili jambo! Ukiamua kulifunga, Mungu atalifunga pia! Anayeanza kufanya kitu ni wewe! Lakini ni lazima ufanye sawasawa na mapenzi yake – la sivyo itakuwa vigumu kwa Mungu kusimama upande wako!
Hivi ndivyo Mtume Petro alivyofanya alipomkuta Yule mtu aliyekuwa kiwete tangu tumboni mwa mama yake – wakati huo alikuwa na umri usiopungua miaka 40 akiomba sadaka katika mlango wa kuingia hekaluni. Mtume Petro alipomwona hakumwomba Mungu amponye bali alimwamuru asimame na kutembea kwa Jina la Yesu Kristo! Alisema hivi, “kwa Jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende”. Halafu; “akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu: (Yule aliyekuwa kilema). Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda, akaingia ndani ya hekalupamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu Mungu.” (matendo ya mitume 3:6-8)
Kile alichoamuru Mtume Petro kitokee kwa Jina la Yesu Kristo kilitokea. Aliamuru Yule kilema asimame na kutembea kwa jina la Yesu Kristo na ikawa hivyo!
Na wewe unaweza kufanya hivyo ikatokea! Kwa nini? Kwa sababu na wewe pia umepewa jina la Yesu Kristo lenye uwezo usiobadilika! Kumbuka Yesu Kristo alisema hivi, “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Labda umeyasoma maneno haya mara nyingi sana kiasi kwamba umeyazoea, na yameanza kuoteza uzito wake kwako. Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa Roho mtakatifu ayahuishe upya ndani yako ili uyaone kama Yeye anavyotaka uyaone.
Siku moja nilikuwa nafundisha neno la Mungu mahali Fulani, na baada ya mafundisho alijitokeza mtu mmoja aliyesema anaumwa kifua na kwamba alihitaji aombewe. Nilimwambia aweke mkono wake kifuani mahali alipokuwa anaumwa – na akafanya hivyo. Na mimi nikaweka mkono wangu juu ya mkono wake, halafu nikasema “kwa jina la Yesu Kristo wa nazareti”! nilipotamka tu jina hili la ajabu, Yule mtu akaanguka chini, na mapepo yaliyokuwa yanabana kifua chake na kuleta maumivu yalianza kupiga kelele. Nikayaamuru yamtoke mtu huyo kwa jina la Yesu Kristo – na yakamtoka wakati huo huo – mtu huyo akasimama akiwa mzima.
Kwa nini ilikuwa hivyo? Kwa kuwa Yesu Kristo alisema kwa jina lake tutatoa pepo! Na ndivyo ilivyo! Tumia mamlaka uliyo nayo, usiogope! Ikiwa wewe ni mwamini yaani umeokoka, jina la Yesu Kristo ni lako – ni uamuzi wako kulitumia au kutolitumia.
Siku nyingine niliitwa kwenda kumwombea mama mmoja ambaye alikuwa hawezi kuinuka kitandani kwa muda wa miezi 2 kwa sababu ya ugonjwa wa homa. Nilipofika katika nyumba hiyo niliweka mkono wangu juu ya kichwa cha maam Yule na kuiamuru homa imwache kwa Jina la Yesu Kristo, kasha nikaondoka. Nilimwacha Yule mama akiwa amelala. Kesho yake mtotowake alikuja kuniambia kuwa mama yake amepona, ameamka toka kitandani na nafanya kazi! Jina la Yesu Kristo libarikiwe milele.
Yesu Kristo alisema tukiweka mikono yetu juu ya wagonjwa kwa jina lake, watapata afya. Na ndivyo inavyotokea tukitii agizo hili. Kuna uweza usiopimika katika jina la Yesu Kristo. Ni ufunguo unaowafungua watu toka katika minyonyoro ya shetani. Usiogope, uwe na moyo wa ushujaa naujasiri mwingi – tumia mamlaka uliyonayo katika jina la Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment