UWEZA WA JINA LA YESU 2.... na Mwl Christopher Mwakasege,

   SURA YA PILI

                     NGUVU UNAYOPATA UNAPOTAFAKARI JUU YA JINA LA YESU KRISTO
“Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana” yoshua 1:8
Mtu mmoja aliwahi kuniuliza swali hili: “Je kutafakari maana yake yake ni nini? Kila mara ninapofundisha somo hili nakutana na swali la jinsi hii.
Naamini kuwa swali hili linawatatanisha wengikwa sababu bado hawajatofaautisha kati ya kusoma neno la Mungu na kutafakari neno.
Kusoma neno ni tofauti na kutafakari neno. Kulitafakari neno no zaidi ya kulisoma neno. Watu wengi huwa wanasoma neno zaidi kuliko kulitafakari.
                                Kutafakari maana yake nini?
Maana ya karibu sana ya kutafakari ni kuwaza. Ni kusoma neno huku unalicheua na kulitafuna rohoni mwako. Kulitafakari ni njia mojawapo kubwa ya kuweza kuilisha roho yako. Yesu Kristo alisema, “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu”. Mathayo 4:4
            Mkate ni chakula cha mwili wan je ulio wa nyama na damu; neno la Mungu ni chakula cha mwili wa kiroho. Kinywa kinapokea chakulana meno yanatafuna na kukivunjavunja huku kikilainishwa na mate, tayari kwa kumeza.
Kusoma neno ni kama kinywa, kazi yake ni kupokea neno.kutafakari ni kuvunjavunja hilo neno huku Roho wa mungu akililainisha liwe tayari kumezwa na roho yako.
Kutafakari neno kunamletea mtu siri ya ajabu yauhakika na ushindi ndani ya Kristo. Sisi ni watenda kazi pamoja na Neno la Mungu hapa ulimwenguni pote. Na kwa sababu hiyo, imeandikwa, “neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu”.( Wakolosai 3:16)
            Huwezi ukawa na neno la kristo moyoni mwako bila kuitumia siri ya kutafakari. Kukariri neno la Kristo hakutoshi peke yake kukuletea uhakika na ushindi kiroho na kimwili kama vile kutafakari kunavyofanya ndani ya mtu.
            Kutafakari ni kuwaza. Kulitafakari jina la Yesu Kristo ni kuliwaza jina hili. Tatizo kubwa sana ambalo linawapata watu ni tatizo la mawazo. Na huu ni ugonjwa mkubwa sana ambao umewakwamisha wengi katika maisha yao ya kiroho.
            Kutafakari na kuwaza ni jambo la rohoni! Si jambo la akili peke yake kama wengi wanavyodhani. Mtu anapowaza uu anapotafakari jambo, huwa ni jambo linalofanyika rohoni mwake.
            Je! Wewe unayesoma somo hili sasa hivi unawaza nini rohoni mwako, unatafakari nini? Mara nyingi utaona mtu anaposoma Neno mawazo yake mara nyingi yanakuwa mbali sana. Kwa hiyo hakuna anachoelewa katika hayo anayosoma.
            Pia, hata wakati watu wanasikiliza neno la Mungu, mara nyingi mawazo yao yanakuwa mbali sana na neno la linalofundishwa. Hii inajidhihirisha hasa ukimwuliza mtu huyo muda mchache baadaye, juu ya neno lililofundishwa maana hatakumbuka.
            Unapoumwa huwa unawaza nini? Wengi wanautafakari ugonjwa, na wengine hata kukata tama anapoona hauponi haraka. Wengine wanapoumwa wanawaza na kutafakari kufa kuliko kuishi. Unapokuwa una matatizo huwa unawaza nini? Unapokosa maelewano na mwenzako, nyumbani, kazini au mahali popote, huwa mawazo yako yanawaza nini? Unapokuwa huna fedha au vitu Fulani vya kimwili huwa unawaza na kutafakari nini?
            Tunaweza kusema mengi lakini swali kubwa ni hili; “kilawakati huwa unawaza nini na kutafakari nini?”
            Je! Unafahamu ya kuwa matendo yako na maneno yako, ni matokeo ya mawazo uliyonayo? Mtu husema anachokitafakari au kukiwaza, na pia hutenda anachokitafakari au kukiwaza moyoni mwake. Ukitaka kumfahamu mtu alivyo rohoni mwake, sikiliza maneno anayosema na nagalia matendo anayoyatenda. Sijaona katika biblia mbapo mtu wa Mungu ameambiwa aitafaari shida yake, awaze juu ya ugonjwa wake.
            Kumbuka kuwa maneno ni chakula cha roho, hali ya roho yako inategemea sana ni maneno gani unayasikia kila wakati na kuyatafakari. Unapotafakari shida, magonjwa, hofu, unaifanya roho yako ijengeke katika hayo. Ukilitafakari jina la Yesu Kristo, roho yako inajengeka katika jina hili.
            Neno la Kristo linakosa nafasi katika roho za watu, kwa sababu roho za watu zimejaa mawazo yanayopinga na kwenda kinyume kabisa na neno la Kristo. Roho ya mtu ni uwanja wa vita. Ukishinda vita katika mawazo, utakuwa umeshinda vita katika mwili, katika roho na katika maneno.
            Wakati mmoja nilianza kujiuliza kwa nini nabii Ezekiel aliambiwa ale gombo la chuo, na mtume yohana aliambiwa ale kitabu kilichofunguliwa.
            Sikuelewa kwa nini hawakusoma tu maneno ambayo yalikuwa yameandikwa bila kula gombo la chuo na kitabu kilichofunguliwa. Mungu alikuwa ana uwezo wa kuwaambia wayasome maneno aliyokuwa anawaonyesha – lakini badala yake aliwaambia wale – kwa nini?
            Nilikuwa siioni tofauti ya kula na kusoma. Kuna tofauti kubwa kati ya kusoma ujumbe wa mungu na kula ujumbe wa Mungu. Soma Ezekieli 2:7; 3:1-3 na ufunuo wa Yohana 10:1-2; 8-11.
            Mtu anapokula chakula, huwa kinatafunwa na kulainishwa kabla ya kumweza. Na kikimezwa na kuingia tumboni, kinanyonywa na kuingia tumboni, kinanyonywa na kuingia katika mishipa ya damu inayozunguka mwili mzima na kukisambaza chakula hicho katika mwili mzima.
            Mtu anapotembea, ukweli ni kwamba ni chakula kile alichokula ndicho kinatembea, INGAWA yeye ndiye anaonekana anatembea.
            Kwa hiyo Ezekieli na yohana walipokula ujumbe wa Bwana uliokuwa umeandkwa katika gombo la chuo na katika kitabu kilichofunguliwa, ujumbe huo uliingia ndani yao kama vile ambavyo wangekula nyama.
            Ujumbe huo uliingia kwenye damu yao na ukajenga misuli. Kila sehemu ilikuwa imejaa ujumbe wa Mungu. Ujumbe huo ndi uliowafanya wapate nguvu  ya kutembea, kuishi na kusema.
            Kwa mtazamo mwingine tunaweza kusema, ezekieli na Yohana walikuwa ni ujumbe wa Mungu uliokuwa unatembea.
            Na sisi tukilitafakari neno la Kristo; na likijaa ndani yetu kwa wingi, tunakuwa ni neno  la Kristo linalotembea, tunakuwa ni neno la Kristo linalosema, tunakuwa neno la Kristo linaloponya.
            Tunafika mahali ambapo kuishi kwetu kunakuwa ni neno(kristo) – kama vile paulo alivyosema “kuishi ni kristo” (wafilipi 1:21). Tukilitafakari jina la Yesu Kristo, tunakuwa ni jina la Yesu Kristo linalotembea… Je! Unauona umuhimu juu ya jambo ninalokuabia la kutafakari?
            Mtu anashindwa kuwa mtendaji wa neno kwa kuwa moyoni mwake hakuna neno. Anabaki kuwa mtendaji wa maneno mengine aliyonayo mawazoni mwake tu – ambayo mengi ni kinyume na neno la Mungu.
 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;  (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo” (2 wakorintho 10:3-5). Hii ina maana kuwa fikra zako ziwaze sambamba na neno( kristo).
Katika kuishi kwetu na kuenenda tuwe tunatafakari nini mioyoni mwetu, ili roho zetu zipate chakula cha kiroho?
            “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo Safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo” (wafilipi 4:8)
Mambo yote haya yaliyotajwa utayakuta katika Neno la Mungu. Kwa kutafakari neno la Kristo usiku na mchana katika mambo yote ndipo utakapoifanikisha njia yako ya Wokovu na ndipo utakapositawi sana kiroho na kimwili.
                Na biblia inasema mtu anayelitafakari neno la Mungu usiku na mchana; anakuwa mtu wa namna hii.
 “Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.” (zaburi 1:3)
            Jina la Yesu Kristo ni la kweli, Jina la Yesu Kristo ni la haki; tena ni safi , tena ni la kupendeza, tena lina sifa njema na nzuri. Tafakari juu ya jina hili usiku na mchana – au waza juu ya jina hili usiku na mchana. Fanya hivyo na wewe utafanikiwa katika kila utendalokwa Jina la Yesu Kristo.
            Unapoumwa usiutafakari ugonjwa, wala kuwaza maumivu yake, bali tafakari neno la Mungu juu ya uponyaji nalo litafanyika afya mwilini mwako. Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote.” (Mithali 4:20-22)
            Unapolitafakari neno la Mungu ndipo unapolihifadhi neno hlo ndani ya moyo wako. Na neno lako Mungu likihifadhiwa ndani ya moyo wako litakuwa AFYA mwilini mwako, na magonjwa hayatakusumbua tena. Hata ikiwa magonjwa yatakujia kukusumbua neno la Mungu lililo ndani yako linakusaidia upate uponyaji.
                Ukilihifadhi neno la Mungu lenye nguvu za uponyaji ndani ya moyo wako utajua hakika ya kwamba “kwa kupigwa kwa (Yesu Kristo) sisi tumepona” (isaya 53:5)
                Wengi wanapata matatizo katika kupokea uponyaji kwa sababu wanaamini kuwa Mungu atawaponya siku moja akipenda kwa sababu wameomba au wameombewa. Hii ni tumaini na siyo imani.
                Imani ya uponyaji huja kwa kusikia na kutenda neno la Mungu linalozungumzia uponyaji. Neno linatuambia ya kuwa tulipona siku nyingi zilizopita kwa kupigwa kwake Yesu Kristo na SIYO tutapona siku moja. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako, magonjwa yanakuwa hayana tena mamlaka juu yako.
                Na ili uwe na uhakika wa afya ya mwili wako kila wakati, inakubidi uwe na tabia ya kulihifadhi Neno la Kristo moyoni kwa kulitafakari.
                Siku moja mtu mmja aliyekuwa anaumwa aliniambia kwa huzuni, “mimi nimeombewa kwenye mkutano wa injili lakini bado sijapona, ingawa niliwaona wenzangu wengi wakisimama kushuhudia kuwa wamepona”.
                Nikamwambia, “na wewe umepona lakini tatizo lako ni kwamba hujui ya kuwa umepona”. Akauliza kwa mshangao, “inawezekana wapi mtu asijijue ya kuwa amepona na huku bado maumivu anayo hata baada ya maombezi?”
                Roho wa Mungu akanionyesha kwa undani zaidi kwa nini mtu huyo alishindwa kupokea uponyaji. Nikamwambia; “uponyaji huwa unapokelewa kwanza katika roho na ndipo unajidhihirisha katika mwili. Wewe ulitaka kwanza uone maumivu yamekwisha ndipo uamini moyoni mwako ya kwamba umepona. Unatakiwa uwe na uhakika kuwa umepona kwa sababu neno la Mungu linasema umepona na siyo mwili unasemaje.”
                Mtu huyo alikuwa na tatizo ambalo watu wengi wanalo. Ni tatizo la kukosa uhakika unaodumu wa kuhusu roho zao na miili yao. Yesu Kristo alisema kwa Jina lake tutatoa pepo, na tukiweka mikono yetu juu ya wagonjwa watapata afya – na ndivyo ilivyo. Amini neno la Kristo alilosema juu ya jina lake na utafanikiwa.
                Neno la Mungu ndiyo kweli inayodumu milele. Neno la Mungu ndilo linalompa mtu uhakika wa jambo ambao hauwezi kuyumbishwa na kitu chochote.
                Neno la Mungu linahifadhiwa ndani ya moyo wa mtu kwa kulitafakari na siyo kwa kukariri peke yake. Mtu anayekariri mistari ya biblia ni sawasawa na mtu anayekula mahindi au chakula cho chote bila kutafuna.  
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote” (wakolosai 3:16)
Kumbuka, Neno la Mungu moyoni mwako ndilo linalokupa uhakika wa mambo yako yote; (Wokovu, uponyaji, ushindi katika majaribu, mamaka yako juu ya shetani na kazi zake, uzima wa milele, na kadhalika)
                Na huo ndio msingi mkubwa wa imani, kwa kuwa “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo…” (Waebrania 11:1)
Kabla imani yako katika Kristo haijaonekana katika matendo yako na maneno yako ni lazima ijengeke kwanza katika moyo wako kwa njia yakulitafakari au kuliwaza Neno la Mungu katika mambo yako yote. 
Matokeo yake ni kwamba utakuwa na uhakika wa jambo lolote moyoni mwako na kwa ajili hiyo utakuwa na ujasiri wa kulisema na kulitenda. Usipokuwa na uhakika wa jamboo moyoni mwako, huwezi ukawa na ujasiri wa kulisema na kulitenda. Neno la Mungu ndilo nuru na taa miguuni petu sisi tulio ndani yake (zaburi 119:105); na kwa sababu hiyo tunaishi katika imani iliyo na uhakika udumuo, na wala si wa kubahatisha.
                Kwa sababu ya umuhimu wa kutafakari neno la Kristo, hapa ninaorodhesha baadhi ya mistari inayozungumzia juu ya jina la Yesu Kristo. Soma maneno yaliyomo na kuyatafakari mara kwa mara na baada ya muda utaona ushindi wa ajabu utakapokuwa unalitumia jina la Yesu Kristo.
                Hakuna Wokovu katika mwingine.
“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”  (Matendo ya mitume 4:12)
“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”(Mathayo 1:21)
“bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” (Yohana 1:12-13)
“Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;
kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.” (warumi 10:12-13)

        Ni amri kuliamini Jina la Yesu Kristo – sio ombi
“Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri.” (1 yohana 3:23)
Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. (yohana 3:18)
      Kuna uponyaji katika Jina la Yesu Kristo
Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
Watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. (Marko 16:17-18)
      “Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa” (yoeli 2:32)

      Lolote ulfanyalo – ulifanye katika Jina la Yesu Kristo.
Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.” (wakolosai 3:17)

Kuomba na kupewa katika Jina la Yesu Kristo.
Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya…… Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. (yohana 14:13-14,26)

“Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” Yohana 16:23-24

            Jina lipitalo kila Jina.
Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;
na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (wafilipi 2:9-10)

Hii ni baadhi tu ya mistari mingi iliyomo katika biblia inayozungumzia juu ya Jina La Yesu Kristo. Waza juu ya jina la Yesu Kristo mara kwa mara na hakika utafanikiwa.

Share:

No comments:

Post a Comment

BABA YUPO NASI

BABA YUPO NASI

Popular Posts

Search This Blog

Recent Posts

Unordered List

  • Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit.
  • Aliquam tincidunt mauris eu risus.
  • Vestibulum auctor dapibus neque.

Pages